Sunday, 19 March 2017

KMPDU wawakataa Madaktari wa Tanzania



Umoja wa Madaktari, Wauguzi na Wataalamu wa Meno nchini Kenya ‘Kenya Medical Practitioners, Pharmacists and Dentists’ Union’ (KMPDU) umepinga vikali hatua ya Serikali ya Kenya kuleta madaktari kutoka Tanzania wakati Kenya ina madaktari wengi ambao hawaajiriwa.

Kupitia kwa Katibu Mkuu wa KMPDU, Ouma Oluga umepinga hatua hiyo na kudai kuwa Serikali ya Kenya haijawa makini katika kushughulika na tatizo la upungufu wa madaktari nchini humo.

Akizungumza na mtandao wa The Star wa nchini Kenya siku ya Jumamosi, Oluga alisema hata hivyo watawakaribisha madaktari kutoka Tanzania na kuwaunganisha katika umoja huo na kwamba watapaswa kupitia mitihani itakayoandaliwa na bodi ya wauguzi.

Amesema mitihani hiyo itachukua sio chini ya miezi mitatu labda kama tu hitaji hilo halitaangaliwa.

“Kenya ina zaidi ya madaktari 1,400 ambao wanasubiria ajira. Itakuwa gharama kubwa na dalili ya kushindwa kutumia fedha za umma vizuri kwa kuwa na madaktari 500 wa kitanzania kwa gharama ya Shilingi 20,000 kwa siku,” amesema.

Oluga amesema kuwa Kenya inapaswa kupitia upya utaratibu wake wa Rasilimali Watu kwa mujibu wa miongozo ya Afya kama ambavyo KMPDU imekuwa ikihitaji hapo kabla.

“Hatuwezi kuwa tunafanyia majaribio maisha ya wakenya katika hali inayoonesha kutowajali wananchi,” ameongeza.


Mapema jana Rais Magufuli alikubali na kuridhia ombi la Serikali ya Kenya na kuahidi kutuma madaktari 500 kusaidia kukabiliana na tatizo la upungufu wa madaktari nchini humo kufuatia mgomo wa madaktari ulioisha hivi karibuni baada ya kudumu kwa siku 100

No comments:

Post a Comment